ads here

HOTUBA YA MGENI RASMI WAZIRI WA KILIMO MH. JOSEPHAT HASSUNGA KUHUSU UZINDUZI WA MKAKATI WA KUENDELEZA ZAO LA MPUNGA AWAMU YA PILI NCHINI, TAREHE 16 DESEMBA, 2019 - KATIKA UKUMBI WA ST. GASPAR ULIOPO JIJINI DODOMA.

advertise here



Ndugu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo;

Wakurugenzi wa Wizara na Taasisi Mliopo;

Wawakilishi wa Wizara za Sekta ya Kilimo;

Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango;

Mwakilishi wa Wabia wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo;

Mwakilishi wa sekta binafsi (TPSF);

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA);

Wawakilishi kutoka Taasisi za HELVETAS, BRiTEN, RIKOLTO na IRRI;

Watumishi wa Umma na Sekta binafsi mliopo;
 
Wawakilishi wa Wakulima;

Wawakilishi wa Wasindikaji wa Zao la Mpunga;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana.

Tumsifu Yesu Kristu!  Asaalam Aleikhum!  Bwana Yesu Asifiwe!

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kupata nafasi hii ya kushiriki nanyi katika uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Zao la Mpunga Awamu ya Pili (NRDS II).

Ndugu Washiriki,
Napenda kuwashukuru waandaaji wa tukio  hili hususan Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ambao wamekuwa nguzo kubwa kwetu katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini ikiwemo maandalizi ya Mkakati huu nitakaouzindua rasmi leo. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa wenzetu wa  HELVETAS, IRRI, BRiTEN RIKOLTO na AGRICOM ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kuweza kufanikisha uandaaji wa Mkakati huu na kufanikisha shughuli ya leo. Niwaombe  muendelee kudumisha ushirikiano uliopo kati yenu na Wizara ya Kilimo katika kufanikisha maendeleo ya kilimo nchini na kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Ndugu Washiriki,
Ikumbukwe kwamba zao la mpunga ni mojawapo ya zao muhimu la chakula  linalozalishwa takribani Mikoa yote hapa nchini. Mwaka 2008, Wizara ya Kilimo iliandaa Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga nchini awamu ya Kwanza (NRDS I). Mkakati huo ulikuwa ni wa miaka 10 na ulitekelezwa na kukamilika Mwaka 2018. Aidha, Mkakati huo ulitoa matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la mpunga kutoka tani 899,000 Mwaka 2008 hadi tani 2,219,628 Mwaka 2018. 

Ndugu Washiriki,
Kama mnavyofahamu, Nchi yetu ina eneo linalofaa kwa kilimo takribani hekta milioni 44.2. Kati ya eneo hilo, hekta milioni 29.4 ni eneo linalofaa kwa umwagiliaji. Hata hivyo, pamoja na kuwa na eneo kubwa linalofaa kwa umwagiliaji, eneo linalotumika kwa sasa kwa umwagiliaji ni hekta 475,052 tu. Hivyo basi, Mkakati huu umekuja wakati muafaka ambao Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Nawasisitiza kuwa, Mkakati huu muutumia kama chombo cha kuhakikisha mnafanya mapinduzi katika zao la mpunga kwa kuongeza eneo la umwagiliaji na kupunguza uzalishaji unaotegemea mvua.

Ndugu Washiriki,
Pamoja na kukamilika kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga (NRDS I) na kuonesha mafanikio makubwa, ni dhahiri kuwa bado tunahitaji kuongeza tija na uzalishaji zaidi. Hii ndo sababu iliyopelekea Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kuandaa Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga Awamu ya Pili (National Rice Development Strategy Phase II - NRDS II) utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi (10) kuanzia Mwaka 2019/20 hadi Mwaka 2029/30.
Lengo kuu la Mkakati huu ni kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pato la wakulima na Taifa kwa ujumla ifikapo Mwaka 2030.
 
Ndugu Washiriki,
Uandaaji wa Mkakati huu ni matokeo ya Mkutano Mkuu wa Coaliation for African Rice Development (CARD) uliofanyika Jijini Tokyo, Japani Mwezi Oktoba, 2018 ambao ulikuwa na malengo makuu mawili ambayo ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa CARD awamu ya kwanza kipindi cha mwaka 2008 hadi 2018 na kuona namna gani awamu ya pili ya Mkakati huo itakavyotekelezwa kwa kipindi cha  Mwaka 2019 hadi 2030.

Ndugu Washiriki,
Mkakati huu wa awamu ya pili unalenga kuimarisha utoshelevu wa chakula nchini, kuchangia utoshelevu wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC), na kuwa  kinara wa soko la mchele katika Jumuiya za Kikanda. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imeweka kipaumbele katika malengo yafuatayo;
Kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mpunga ambazo zinastahimili ukame na kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za uzalishaji zitakazo himili mabadiliko ya tabia nchi;
Kupunguza gharama za uzalishaji na kuweka mifumo bora ya udhibiti ili mchele wetu uweze kushindana kwa bei na ubora na michele inayotoka nje ya nchi.
Kuimarisha mifumo ya uzalishaji na masoko hususan kwa wakulima wadogo ili kukifanya kilimo cha zao la mpunga kuwa endelevu na kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi; na
Kuongeza eneo la kulima zao la mpunga katika maeneo ya umwagiliaji na yanayotegemea mvua. Pia, kuimarisha na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kuwajengea uwezo wakulima kuhusu usimamizi wa miundo mbinu hiyo.

Ndugu Washiriki,
Ili kufikia malengo niliyoanisha hapo juu, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa zao la Mpunga nchini tutatekeleza yafuatayo;
Kuongeza eneo la uzalishaji wa mpunga kutoka hekta milioni 1.1 za mwaka 2018 hadi hekta milioni 2.2 ifikapo mwaka 2030;
Kuongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa tani 2.2 kwa hekta hadi kufikia wastani wa tani 4.4 kwa hekta ifikapo mwaka 2030;
Kuongeza thamani ya zao la mpunga kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni pamoja na kupunguza upotevu kabla na baada ya mavuno; 
Kuimarisha mifumo ya masoko na kilimo biashara; 
Kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mpunga pamoja na kuimarisha mifumo ya mbegu;
Kuongeza upatikanaji wa mbolea kwa kuanzisha Viwanda vya kuzalisha na kuchanganya mbolea nchini ikiwa ni pamoja na mifumo ya masoko na usambazaji;
Kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuhamasisha teknolojia za umwagiliaji zinazotumia maji kwa ufanisi; na
Kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani na kuboresha mifumo ya masoko na upatikanaji wa mitaji.

Ndugu Washiriki,
Nimefarijika kwa kazi nzuri iliyofanywa hasa ambavyo mmeweza kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambao ndio Wadau wakubwa katika kutekeleza Mkakati huu. Niwatake wadau wote wa zao la mpunga nchini mtambue kuwa Wizara ya Kilimo itashirikiana nanyi ili kuweza kutekeleza mkakati huu na kufikia malengo tuliojiwekea.

Ndugu Washiriki,
Nimearifiwa kuwa Mkakati huu kwa sasa umeandaliwa kwa lugha ya Kiiengereza. Nichukue fursa hii kuwaomba Wadau mbalimbali muweze kushirikiana na Serikali ili kuweza kutafsiri Mkakati huu kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kufanya hivyo, kutapelekea kuwafikia walengwa wengi zaidi ambao wengi wao wanazungumza kwa ufasaha lugha yetu ya Taifa Kiswahili.

Ndugu Washiriki,
Naomba niendelee kuwasisitiza ndugu zetu wa JICA, HELVETAS, IRRI, RIKOLTO, BRiTEN, AGRICOM na Wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati huu ambao umeanisha viashiria chanya vya kuendeleza zao la mpunga; na hatimaye kuifanya Nchi yetu kuwa mzalishaji na soko kuu la mchele katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika. 

Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kuwa Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Zao la Mpunga awamu ya pili (NRDS II) umezinduliwa rasmi. 
 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Advertisement
BERIKAN KOMENTAR ()